HIVI NDIVYO MAISHA YALIVYO!

Tuesday, September 12, 2006

Msangi umekuwa kamanda anayechagua pori?

Ni hivi tu, aaaa anyway

natumai watu wote mu wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu ya kikazi hasa katika dunia hii iliyojaa mbwembwe, majigambo, kujisifu na hata aaa yaani hali ya watwawala wetu aa sorry naamanisha watawala wetu wanavyotulaghai kwa maneno mataam na si wenyewe tunakubali tu si tumezoea.

Nasema haya nikikumbuka tukio lililotokea mapema mwezi huu huko wilayani Mbozi katika mji mdogo wa Tunduma ambao unakuwa kwa kasi katika masuala ya kibiashara.

Kwa wasioifahamu wilaya ya Mbozi ina vijisifa kiasi, ingawa havipendezi masikioni, kwa mfano uchunaji wa ngozi za binadamu pamoja na utangenezaji wa silaha haramu maarufu kama magobole ambayo yanatumika katika uhalifu hawa jamaa ni stadi kwa hilo, sasa sijuin kwanini utaalamu wao wa kutengeneza silaha hauboreshwi, lakini hilo la ngozi inafaa lilaaniwe kwa nguvu zote.

Katika tukio la Tunduma, mtanzania mmoja aliyejulikana kwa jina Lucas Msuya alimaarufu mangi aliuawa kwa kupigwa na polisi wa Zambia kwa kile alichodaiwa kuwa ni kununua mali za wizi.

Kama kawaida vyombo vya habari vya ndani na nje vilihamasika kwa kiasi kikubwa kuipata habari hiyo kwa kuwa ilikuwa ni ishu ya kimataifa.

Kwa hili sitasita kuwapongeza waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya kwa jinsi walivyojitahidi kufuatilia na kuripoti matukio yote yaliyokuwa yanatokea huko na kuwafanya watanzania wote wawe makini na kujua hali halisi ya kinachojiri Mkoani Mbeya hususani katika mji wa Tunduma.

Ngoja niwapongeze hawa walifanya kazi kubwa kweli kweli, Ramandani msangi, Rashid Mkwinda,solomoni Mwansele aaa ni wengi hao ni kwa uchache kwa kweli walifanya kazi nzuri.

Haikuishia hapo bwana msangi akapandisha habari yake nzuri kabisa katika blog, ikieleza jinsi mkuu wa kaya ya Mbeya alivyokuwa akiongea na wakazi wa tunduma kuelezea kile alichoongea na maafisa wa serikali ya zambia.

Ilidaiwa kuwa Mkuu huyo wa kaya ya Mbeya,Tunduma ikiwa ndani yake alitamba kuwa watanzania wamechoka kunyanyaswa, akasema zaidi kuwa serikali ya zambia imekiri kuhusika na mauaji hayo na tamu zaidi ni kwamba imeundwa tume itakayochunguza chanzo cha vurugu hizo pamoja na timu ya Madaktari wa tanzania na Zambia wataoufanyia uchunguzi mwili wa marehemu msuya au mangi.

Akaja naye Mkuu wa polisi, huyu alijifaragua kuwa hawatavumilia kuona watanzania wananyanyaswa wakiwa ndani ya nchi yao na nje ya nchi,huku akiwata wananchi watulize mzuka na kuiachia serikali ichukua hatua zaidi kuhusiana na suala hilo.

Kweli waandishi hao baadhi niliwataja na wengine walifanya kazi kubwa kuufahamisha umma wa tanzania tangu mwanzo wa tukio hadi kauli hizo zao wanaotungoza kwa kasi kuelekea maisha, ambayo tunaambiwa ni bora huku matatizo yakiongezeka kila kukicha hususani umeme, lakini nasikia mwezi octoba kuna mvua ya kutengeneza itaanza kunyesha kwa malipo ya tushilingi milioni mbili, Waziri Mkuu amesema eti hizo ni hela kidogo tu, mi sina hakika kama ni kweli.

Aaaa tuyaache hayo, lakini ikiwa ni takribani wiki mbili sasa nilikuwa nasubiri baada ya Msangi na timu ya wenzake kingefuata nini naona wapo kimya, sidhani kama ndio habari ya Tunduma wameachana nayo, aaa sijasema hivyo labda wanatafakari waanze vipi, sidhani kama wanataka watoke vipi maana walikwisha toka.

Labda wakati wanatafakari wajaribu kuyaona haya, hivi familia ya mangi imelipwa fidia gani kutokana na mauaji hayo ya makusudi, lakini bado najiuliza huku nikiwa na shaka shaka moyoni, inadaiwa marehemu huyu alikabidhiwa na polisi wa tanzania kwa polisi wa Zambia ambao baadae walitoa kipigo kikali na kusababisha kifo cha kijana huyu ambaye ni nguvu kazi ya Taifa loo masikini natumai bado taifa lilikuwa linamuhitaji.

Nilisikia polisi wawili wa Zambia wanaodaiwa kusababisha kifo hicho hicho walitiwa korokoroni na baadae kufikishwa mahakamani, sasa sijajua nini hatma ya wale askari walimuweka chambo kijana huyo kushindwa kufuatilia kujua nini kinampata kijana huyo wa Kitanzania ambaye ni mwenzao tatizo ni moja tu hakuwa askari labda ndio maana walimsahau.

Pamoja na hayo hiyo ripoti sijajua inangoja nini, Msangi, Mkwinda na wengine waandishi mliopo Mbeya vipi mbona kimya tulitaraji kuona mfululizo wa habari za tunduma ili nasi tukae huku tukiwa tumejibweda na kumwaga stori za tunduma kana kwamba tupo tunashuhudia kumbe nyie mnacheza heko ya kutuhabarisha.

Msilale tupeni mambo au Mmekuwa makamanda wanaochagua pori???
Sitaki kuamini hilo
tchao

Monday, May 29, 2006

Hivi misukosuko hii mpaka lini kwa vijana?

KURUNZI LANGU MCHAMBUZI

Hivi misukosuko hii mpaka lini kwa vijana?

Julai mwaka jana, Serikali Tanzania, iliamua kuzipandisha hadhi Halmshauri za Manispaa kadhaa na kuzifanya kuwa Halmashauri za majiji hivyo kujikuta kuwa Nchi yetu ina majiji matano, tofauti na mwanzo ambapo kulikuwepo na majiji mawili tu.

Miongoni mwa majiji hayo ni pamoja na Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga na Mbeya ambalo limekuwa ni Jiji linalobadilika kwa kasi ikiwa ni pamoja na kukua kwa biashara na kuboreshwa kwa miundo mbinu.

Katika kuchukua hatua za kuyaboresha majiji hayo, Halmashauri zilianza kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza mapato yake kwa kujenga mifumo imara wa ukusanyaji mapato, kuanzisha vituo vya matangazo ya redio na luninga, kuboresha miundo mbinu ya barabara na mawasiliano.

Hatua hiyo imekwenda sambamba na upigaji marufuku kwa shughuli za vijana kama zinazo husisha mikokoteni kuendeshwa katika barababara kuu za Halmashauri ya Jiji, kuhamishwa kwa wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ katika maeneo ya katikati ya jiji, madereva taksi kutakiwa kuacha kuegesha magari katika maeneo yasiyo rasmi.

Kupigwa marufuku kwa mikokoteni katika barabara kuu kulitokana na ukweli kwamba mikokoteni imekuwa ikisababisha ajali, vifo na uharibifu wa mali kutokana na waendeshaji wake kutokuwa makini, wakati wamachinga wametakiwa kuondolewa katika maeneo waliyozoea kufanya biashara zao kupisha kuanzishwa kwa biashara nyingine yakiwemo mabenki.

Mabadiliko ya kasi yanayoendelea kutokea yamekuwa yakionyesha athari za wazi kwa vijana, ambapo kutokana na ukosefu wa elimu na ajira, vijana wengi wamejiajiri katika shughuli za nguvu kazi pamoja kufanya biashara ndogondogo kwa lengo la kujipatia kipato kinachowawezesha.

Kutokana na kujishughulisha na kazi ndogo ndogo vijana wengi waliepuka kushiriki katika vitendo viovu ukiwemo uhalifu mdogo mdogo, uporaji pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, pamoja na kuchukua hatua mbalimbali zenye manufaa ya kuyaboresha majiji hakuna, juhudi za dhati zinazowaandaa vijana kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea ikiwa ni pamoja na kuwaandalia shughuli na maeneo mbadala.

Nionavyo mimi, Halmashauri ya Jiji la Mbeya inapaswa kuanza kuchukua hatua za kuwaandaa vijana kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea kutokea ili vijana wawe tayari kukabiliana na mabadiliko yanayotokea.

Ni muhimu kabla ya Halamshauri haijapiga marufuku uendeshaji wa mikokoteni, kuwahamisha wamachinga pamoja na madereva taksi ikachukua hatua ya kuwaelimisha na kuwatafutia maeneo mbadala ambayo yatakuwa na tija katika uendeshaji wa shughuli zao.

Kwa kutoa matangazo yanayonukuu vipengele vya sheria katika kupiga marufuku aina mbalimbali za shughuli zinazoendeshwa, haiwawezeshi vijana kuamini tofauti na wanachoamini kuwa kinachofanyika ni aina mojawapo ya unyanyasi kwa vijana hawa wasio na sehemu ya kukimbilia.

Wapo vijana wanaodai kuwa wamefanya kazi ya mikokoteni kwa zaidi ya miaka 10, wapo madereva taksi waliofanya kazi katika kituo kimoja kwa zaidi ya miaka 20 na wamachinga wanaofanya biashara katika maeneo mbalimbali kwa muda mrefu bila ya kuwa na mabadiliko ya ghafla yanayoendelea kutokea.

Kwa kupiga marufuku na kuainisha vipengele vya sheria vinavyohalalisha upigaji marufuku huo haitoi fursa za kusaidia, bali kuathiri jamii hii,jambo ambalo si stahiki yao, Halmashauri zinahitajika kuwaanda vijana kukabiliana na mabadiliko yanayotokea ili wasione kuwa ni mambo mageni.

Kwa kuwakatia mianya inayowaingizia kipato halali vijana bila kuwatafutia njia mbadala, Halmashauri inakuwa haijawasaidia vijana kwa kuwa kutokana na wengi kukosa uwezo wa kiuchumi wanashindwa kubuni miradi mingine itakayowawezeshwa kukupata kipato halali.

Halmashauri zinachangamoto ya kuwatambua vijana na aina za ajira zisizo rasmi wanazofanya, hii itaisaidia Halmashauri za majiji kuweka mipango thabiti ambayo haitawaathiri vijana ikiwa ni pamoja na kuwatafutia shughuli mbadala.

Kadhalika Halmashauri inatakiwa kuchukua juhudi za makusudi za kuwaelimisha vijana waungane katika vikundi, watambue fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo wanayoishi ili waweze kuachana na shughuli ambazo hazitakiwi kuendeshwa katikati ya jiji.

Hata hivyo vijana wanatakiwa kutokata tamaa na kuacha kutumia njia za mkato katika kujipatia kipato ikiwa ni pamoja na kushiriki katika vitendo vya uhalifu, uuzaji na utumiaji wa dawa za kuelevya pamoja na biashara ya ukahaba.

Kwa muono wangu sasa mapambano ndio kwanza yameanza Halmashauri hizi za majiji zikianza zikiwaondoa vijana eti zinataka kuweka Bank basi vijana waseme wanataka kuweka SACCOS ili tuone uzalendo wa Halmashauri zetu kwa vijana pia.

Nilikuwa nanyi, nipo nanyi na nitakuwa nanyi katika uchambuzi wa mambo.

Alamsiki!

Monday, May 15, 2006

Hivi ndivyo maisha yalivyo ndio ujio wangu, hivi ndivyo nitokavyo katika kijiwe hiki ambacho kwa hakika, lengo la kijiwe hiki ni uchambuzi wa mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, nk

Natumai tutashirikiana kwa pamoja kurudisha heshima ya wachambuzi wa mambo ile ya iliyokuwepo awali ambayo kamwe haiwezi kusahauliwa mengi tutayapata, mengi tutayajua na kuyajadili kwa pamoja!